SAKATA la usajili wa mshambuliaji wa
Mbeya City, Saady Kipanga, kwenda Simba, limechukua sura mpya baada ya viongozi
wa klabu hiyo kushindwa kuelewana kwa maelezo kwamba kigogo mmoja amemsajili
kibabe bila wenzake kuridhia.
Awali viongozi wa Kamati ya Usajili
kwa ushirikiano na viongozi wengine wa Simba, walikubaliana kufuta usajili wa
mchezaji huyo. Lakini baadaye mmoja wa vigogo hao (jina tunalo) aliliibua suala
hilo upya juzi Jumatano kwa madai kuwa tayari amemsainisha Kipanga mkataba wa
miaka miwili.
Siku hiyo kamati hiyo
ilikutana kujadili mustakabali mzima wa usajili na kufunga kazi hiyo ili kocha
apate muda wa kukaa na wachezaji husika, lakini ishu ya Kipanga ikatibua uelekeo
wa kikao. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zacharia
Hans Poppe.
Suala hilo lilionekana kuwagawa
baadhi ya wajumbe wa kamati ambapo walio wengi walionekana kupinga juu ya
usajili huo huku wajumbe watatu pekee wenye ushawishi wa kifedha wakiunga
mkono. Wajumbe wengi walikuwa wakimtaka Elius Maguli ambaye yupo kwenye orodha
ya matakwa ya kocha.
Mbeya City watoa tamko
Uongozi wa Mbeya City umesema kuwa
ulipokea barua ya kiongozi mmoja wa juu wa Simba juu ya maombi ya usajili wa
Kipanga, Deus Kaseke na Anthony Matogolo na kuwapa masharti ya kutimiza.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel
Kimbe, alisema baada ya kuijibu barua hiyo ya Simba, hawakupokea mwendelezo
wowote wa mawasiliano juu ya usajili hivyo wanashangaa kusikia Kipanga kasajiliwa
Simba wakati bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo na kama ni
kweli watashtaki.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni